Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah “Try Again” amesema klabu hiyo haina hofu na timu yoyote Barani Afrika na ipo tayari kucheza popote na kuonesha upinzani.
Try Again ametoa kauli hiyo baada ya Simba SC kupangwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kiongozi huyo amesema Simba SC imejizatiti Kimataifa na ina uzoefu wa kutosha, hivyo Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wanapaswa kukiamini kikosi chao kuelekea mchezo huo.
Amesema jambo la muhimu kwa Uongozi, Benchi la Ufundi na Wachezaji wa Simba SC ni kujiandaa vizuri kuelekea mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini Tanzania na Afrika Kusini.
“Kwa ukubwa wa Simba sasa hivi hatuna sababu ya kuhofia timu yoyote kwani ni klabu gani kubwa ambayo Simba hatujakutana nayo? Kwetu hakuna kipya tena chini ya jua, kitu muhimu kwetu ni maandalizi bora na kujipanga.” Amesema Try Again.
Mchezo wa mkondo wa kwanza utachezwa Dar es salaam-Tanzania, Uwanja wa Benjamin Mkapa kati ya April 15-17, huku mchezo wa Mkondo wa pili ukitarajiwa kupigwa Afrika Kusini kati ya April 22-24.
Simba SC ilitinga Robo Fainali kwa kishindo Jumapili (April 03), kwa kuifunga USGN ya Niger mabao 4-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ushindi huo uliifanya Simba SC kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D kwa kufikisha alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco, ikizidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.