Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky Ijumaa anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen mjini Kiev.

Msemaji wa rais wa Ukraine, Sergii Nykyforov amesema kuwa taarifa zaidi kuhusu mkutano huo hazitotangazwa kutokana na sababu za kiusalama.

Naye Msemaji wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell anatarajiwa kufanya ziara katika mji wa Kiev mapema wiki hii.

Borell amesema awamu mpya ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa Urusi ikiwemo marufuku ya mauzo ya mkaa, huenda ikakubaliwa ifikapo Ijumaa.

Akizungumza na waandishi habari, Borell amesema umoja huo utajadiliana kuhusu vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi ifikapo siku ya Jumatatu.

Huku hayo yakijiri, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajia kupiga kura iwapo iisimamishe Urusi uanachama katika Baraza la Haki za Binaadamu la umoja huo.

Kura hiyo imependekezwa na Marekani kutokana na madai kwamba wanajeshi wa Urusi waliwaua raia wakati wakiondoka kwenye mji wa Bucha, ulio karibu na mji mkuu, Kiev.

Msemaji wa Baraza la Umoja wa Mataifa Paulina Kubiak amesema kikao maalum kuhusu Ukraine kitafanyika Alhamisi na azimio hilo litapigiwa kura. Ili Urusi iweze kusimamishwa uanachama, panahitajika theluthi mbili ya kura zote bila kujumuisha wajumbe ambao watajizuia kupiga kura.

Wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu lenye wanachama 47 wanachaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa vipindi tofauti vya miaka mitatu. Muhula wa Shirikisho la Urusi unamalazikika mwaka 2023, kama ilivyo kwa Ukraine.

Wanafunzi wafariki kwa mshtuko wa moyo
Rais Wa Zambia anahudumu bila kulipwa Mshahara