Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda amesema uchanga wa baadhi ya wachezaji wake umechangia kupoteza mchezo dhidi ya Simba SC leo Alhamis (April 07).
Coastal Union ilikua nyumbani Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga kuikabili Simba SC iliyofunga safari kutoka Dar es salaam.
Mgunda ambaye amekabidhiwa jukumu la kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi siku kadhaa zilizopita, amesema wachezaji wake walikua makini kuikabali Simba SC, lakini dakika za mwisho walishindwa kujipanga kutokana na kuwa na uzoefu mchanga.
“Napongeza wachezaji wangu wamecheza vizuri, wameonesha kuna kitu wamejifunza tangu niliporudi, lakini kilichowaangusha hadi kupoteza mchezo ni uchanga kwa baadhi yao.”
Ukiangalia bao tulilofungwa dakika za mwisho, mpira ulikua kwetu lakini mchezaji wangu akataka kuvuka nao upande wa pili kwa kukimbia ili hali alikua amechoka, kilichotokea wenzetu waliupata mpira na kupiga pasi ndefu na hatimaye tukafungwa bao lililotufanya tupoteze mchezo.” amesema Juma Mgunda
Kiungo Mkabaji kutoka Nigeria Victor Akpan aliisawazishia Coastal dakika ya 76 kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja na kumuacha Aishi Manula.
Akitokea benchi Mshambuliaji hatari Meddie Kagera alipigilia msumari wa pili dakika ya 90+2 kwa bao safi huku Coastal walipata pigo dakika ya 87 kwa beki wake Patrick Kitenge kuonyesha kadi nyekundu.
Kwa ushindi huo Simba wamefikisha alama 40 zinazoiweka nafasi ya pili huku Coastal Union wakibaki nafasi ya 12 wakiwa na alama 21.