Uongozi wa Mtibwa Sugar umeshindwa kusema lolote kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Beki wao Mzawa Abdi Banda anayedaiwa kufanya mahojiano na chombo cha habari cha Afrika Kusini na kutoa kauli za kuichafua Simba SC.

Abdi Banda ambaye aliwahi kuitumikia Simba SC kabla ya kutimkia Afrika Kusini anadaiwa kufanya mahojiano hayo na Jarida la Kickoff Magazine la Afrika Kusini na kuitahadharisha Orlando Pirates kuwa makini itakapokuja nchini kucheza mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali, Kombe la Shirikisho.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Mtibwa Sugar, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Thobias Kifaru amesema kazi yake ni kuisemea klabu kupitia vyombo vya habari na sio kumsemea mtu mmoja.

“Mimi sio msemaji wa Mtu mmoja bali mimi msemaji wa Taasisi ya Mtibwa Sugar na ndio maana naruhusiwa kuizungumzia taasisi yangu ya Mtibwa na hivi sasa Abdi banda tupo nae kambini na kikosi cha Mtibwa kitaendelea na mazoezi katika dimba la Manungu” amesema Kifaru

Abdi Banda anadaiwa kusema: “Orlando Pirates wanapokuja Dar es Salaam, lazima watarajie kukutana na vitendo vichafu na wajue kwamba vita itakuwa nje ya mpira kwa sababu Simba anaungwa mkono na wanasiasa.”

“Simba watabebwa na mwamuzi kwa sababu watampa fedha. Simba utumia mbinu chafu wanapocheza nyumbani, lakini kiukweli hawana Ubora ambao Pirates anao na ili waweze kufuzu watajipanga kupata ushindi mkubwa nyumbani.”

Simba SC itacheza dhidi ya Orlando Pirates Jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mchezo wa Mkondo wa Pili ukipangwa kuchezwa April 24 Afrika Kusini.

Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kufanyika Agosti 23
Ibenge amtabiria makubwa Fiston Mayele