Mwanamume aliyepondwa na kuchemshwa hadi kufa katika tanuri ya kampuni ya Blue Nile Rolling Mills mjini Thika amezikwa jana nyumbani kwao eneo la Kogony katika Kaunti ya Kisumu mnano Jumamosi, Aprili 9.
Mabaki ya Caleb Otieno yaliondoka katika hifadhi moja ya maiti mjini Thika mnamo Ijumaa na kusafirishwa hadi nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi.
Otieno alikuwa na kibarua cha kuweka vipande vya chuma katika moto mkali na siku ya kufa kwake mnano Machi 25, alikuwa kazini kama kawaida na taarifa zinasema dakika chache kabla ya kifo chake, alimpa mwenzake pesa ili amnunulie chakula cha mchana na aliporudi na Ugali, mboga, pojo zilizochemshwa na maharagwe, Otieno hakuwepo tena.
Inaelezwa kuwa alipokuwa akiweka vipande vya chuma kupitia kinu cha kuviringisha kwenye tanuri inayowaka, vishika mikono vyake vilikwama kwenye vyuma na ndipo vinu vilipomvuta kwenye mashine ambayo ilimponda vipande vipande kabla ya kumwangusha katika tanuri.
DCIO wa kaunti ndogo ya Thika Joseph Thuvi aliliambia gazeti la the Star kuwa walifika eneo la mkasa na kukusanya chembechembe ambazo zilionekana kuwa vipande vya mifupa kutoka kwa tanuri hilo na kuwa suala hilo litashughulikiwa tu kama tukio Ła ajali za kawaida kazini.
Taarifa zinasema kuwa kampuni hiyo imeiambia familia ya Otieno kwamba itakuwa ikiwalipa pesa kila mwezi kwa miaka mitano kama fidia.