Mabingwa watetezi Tanzania Bara Simba SC wameshindwa kuwika katika Uwanja wa Ushirika Mkoani Kilimanjaro dhidi ya Polisi Tanzania waliokua wenyeji leo Jumapili (April 10).
Simba SC imemaliza dakika 90 za mchezo huo kwa matokeo ya sare ya bila kufungana huku Polisi Tanzania wakipata nafasi nyingi za kufunga lakini walishindwa kufanya hivyo.
Upande wa Simba nao walifanikiwa kufika mara kadhaa katika lango la Polisi Tanzania, lakini nafasi walizozipata zilikuwa tofauti na zile za wenyeji wao.
Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amesema hana budi kuwapongeza wachezaji wake japo eneo la kuchezea la Uwanja wa Ushirika halikua rafiki.
“Nashindwa kuuita mchezo huo ni soka, kwa kweli ni vigumu kucheza hapa na kusema umecheza soka, lakini yote kwa yote tunapaswa kukubali matokeo na kuangalia michezo iliyo mbele yetu.” Amesema Kocha wa Simba Franco Pablo Martin
Naye Kocha Msaidizi wa Polisi Tanzania George Mketo amesema wamefanikiwa kuibana Simba SC katika dakika zote 90, kufuatia wachezaji wao kufuata maelekeo waliowapa.
“Tuliitazama Simba SC na tukafahamu wangetumia mipira mirefu na sehemu za pembeni, tuliwaeleza wachezaji wetu na wamefanikiwa kuwabana, na tumepata matokeo ya sare.” amesema Kocha Msaidizi Mketo.
Kwa matokeo hayo Simba SC inafikisha alama 41 ambazo zinaendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 51.
Polisi Tanzania inafikisha alama 24 zinazoiweka timu hiyo katika nafasi ya 08.