Kwa zaidi ya wiki mbili mfululizo moja ya habari kubwa kumuhusu nyota wa muziki wa bongo fleva Rajab Kahali maarufu Harmonize ni kuhusu kurudi kwenye uhusiano wa kimapenzi na muigizaji Kajala Masanja.

Suala hilo limezua mjadala mkubwa hasa likiwashangaza wadau mbali mbali kutokana na namna ambavyo msanii huyo amekuwa akiweka wazi hisia zake kwenye mitandao ya kijamii kwa mfululizo wa machapisho yenye maneno mazito.

Jambo hilo limewafanya baadhi ya mashabiki kuhoji athari za vitendo hivyo na hata kuuliza “wapi ulipo uongozi wa msanii huyo” na “kwanini wanamuachia anafanya vitu vyenye taswira ya kujidhalilisha” licha ya kuwa hapo awali Harmonize aliachana na Kajala kwa sakata zito.

Baada ya maswali yote hayo hatimaye uongozi wa msanii Harmonize umetolea ufafanuzi suala hilo kupiti kwa mmoja wa mameneja wa msanii huyo aitwaye Mchopa.

“Situation ya Harmonize ni ya kawaida ambayo watu wengi huwa wanaipitia  kwa hiyo sisi menejimenti hicho sio kitu kigumu ku-control kwa sababu haiathiri ufanyaji wake wa kazi, anafanya kazi na vyote vinaenda.” Amesema Mchopa.

Mchopa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na mtangazaji Mammy Baby kwenye kipindi cha Top20 kupitia Cloudsfm.

Licha ya kupaza sauti akimuomba msamaha muigizaji Kajala Masanja ili warudiane, bado mambo yameendelea kuonekana kuwa magumu kwa msanii Harmonize ambaye siku chache zilizopita Kajala alimblock kwenye mitandao ya kijamii akidhihirisha wazi kuwa hayuko tayari kurudia na nyota huyo.

Ruby atamani 'kifo'
Young Africans yatangulia Nusu Fainali ASFC