Zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi na Postikodi katika Wilaya ya Kinondoni limeendelea kwa ufanisi tangu lilipozinduliwa rasmi kwenye wilaya hiyo tarehe 18 Februari, 2022 ambapo Kinondoni kati ya wilaya nyingine za Dar es Salaam imefanikiwa kwa kufikia asilimia 95 mpaka sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe ameeleza kuwa Kinondoni imekuwa na muitikio mkubwa kwenye zoezi zima la Anwani za Makazi na Postikodi ambayo ni chachu ya maendeleo ya pamoja na binafsi na hilo limewezekana kufuatia utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa Anwani za Makazi na Postikodi kuanzia ngazi ya chini ya Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Mitaa, Maafisa Tarafa, Mabaraza ya Madiwani na wataalamu wanaoendesha zoezi zima hadi kufikia ngazi ya kaya kwa wakazi wa Kinondoni.
”Tulitaka wananchi waweze kufahamu na waweze kuitikia kwa hiari ili walichangamkie na walifurahie zoezi la Anwani ya Makazi na Postikodi. Zoezi linaendelea vizuri na tunafahamu umuhimu wake na tunajua kwamba hii ni moja ya fursa kubwa sana kwetu. Tumeshajipanga tayari na kazi ilishaanza muda mrefu. Tulianza kwanza kwa kutoa elimu ili wananchi wa Kinondoni waweze kuelewa umuhimu wake kwa maisha yetu ya kila siku,”ameeleza Mhe. Gondwe.
Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Hanifa Suleiman Hamza amesema kuwa Manispaa hiyo ya Kinondoni yenye Postikodi namba 14000 ambayo imeundwa na Tarafa 2, kata 20 na mitaa 106 ina takriban ya watu 926,681 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 na idadi inatarajiwa kuongezeka kufikia watu 1,514,000 ifanyikapo sensa ya mwaka huu 2022/23.
“Mpaka sasa Wilaya yetu ina takriban nyumba 135,942. Kati ya nyumba hizo nyumba 45,070 sawa na asilimia 33.1 zimeshawekwa kwenye mfumo. Kwa ujumla nyumba zote za Kinondoni zimefanikiwa kupewa namba za nyumba ambapo wakusanya taarifa wameshapita kwenye kila kaya kukusanya taarifa za wakazi wote hivyo zoezi zima la uandikishaji limefikia asilimia 95 mpaka sasa,” ameeleza Bi. Hanifa.
Katika Wilaya ya Kigamboni zoezi hilo limeendelea na hadi sasa likiwa limefikia asilimia 84.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, James Mkumbo ameeleza kuwa Kigamboni ambayo ina Tarafa tatu za Somangila, Pemba Mnazi na Kigamboni, Kata 9, Mitaa 67 na wakazi wapatao 238,591 imeendelea na zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi kwa ufanisi mkubwa ambapo mpaka sasa kata 6 kati ya kata 9 zimefikiwa.
“Eneo kubwa la Manispaa ya Kigamboni ambalo ni 70% ya eneo zima limepimwa hivyo imeongeza ufanisi mkubwa wa utekelezaji wa zoezi hili hasa katika hatua ya kuzitambua nyumba na eneo zilipo, wapi zoezi linapaswa kusogezwa na kutambua maeneo ambayo hayajaendelezwa ili kuchochea maendeleo katika maeneo hayo.
Kwa kutumia kikosi kazi maalum cha wataalamu 11 wa kusoma ramani maeneo yote yametambulika na taarifa zimeendelea kuchukuliwa bila kuacha mtu nyuma” ameeleza Bw. Mkumbo.
Amesema kuwa hadi sasa kaya 41,540 zimefikiwa katika uwekaji wa namba za nyumba sawa na asilimia 84 ya zoezi zima ambapo mkakati uliopo ni kukusanya taarifa takriban nyumba 3,000 kwa siku huku lengo kuu likiwa ni kuzifikia kaya 49,353 kwa ujumla.
“Uwekaji wa taarifa hizo za wakazi kwenye kanzidata unaendelea na umefikia asilimia 26 na kwamba zoezi hilo linaendelea kuboreshwa ili kuwafikia wakazi wote wa Kigamboni na hatimaye zoezi hilo kukamilika kwa 100% ifikapo Mei 2022”, amesisitiza Mkumbo.
Uwekaji wa Anuani za Makani na Postikadi umekua ukiendelea nchin nzima katika miji na majiji kwa lego la kurahishisha zoezi la sensa ya watt na Makani inayotarajia kufanyika mwezi agosti 2022.