Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na timu yake leo Jumatatu April 11, 2022 wameanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kufanya uhamasishaji wa uwekaji anuani za makazi.
Akiwa Uwanja wa ndege jijini Dodoma wakati anaanza safari, Nape ameitaja mikoa ya Tanga na Dar es Salaam kuwa bado haijafanya vizuri kwenye uwekaji wa anuani za makazi.
Waziri Nape amesema shughuli hiyo ya uwekaji wa anuani za makazi nchini inatakiwa kuhitimishwa Mei 22, 2022 ingawa kwa sasa imefikia wastani wa asilimia 68 kwa nchi nzima.
Leo Waziri huyo akiwa na timu yake wameanzia ziara hiyo mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha na amesema katika baadhi ya maeneo wanalazimika kuongeza nguvu kupeleka wataalamu zaidi.