Shrikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limetangaza kuwa na mpango wa kutembelea viwanja vyote vitakavyotumika kwa michezo ya hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa barani humo.
‘CAF’ wamepanga kukagua viwanja hivyo sababu Teknolojia ya usaidizi wa picha za video kwa waamuzi (VAR) kwa msimu huu itaanza kutumika kuanzia Michezo ya Robo Fainali na sio Michezo ya Fainali pekee kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Jijini Dar es salaam Tanzania, ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumika, kufuatia Simba SC kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho.
Simba SC itacheza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika Uwanja wa huo Jumapili (April 17), na teknolojia ya usaidizi wa picha za video kwa waamuzi (VAR) itatumika kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hata hivyo imeelezwa kuwa ziara ya maafisa wa CAF katika viwanja vitakavyotumika kwa Michezo ya Robo Fainali, kukagua uwanja utaokuwa bora kwa viwango vya teknolojia hiyo, ili kutoa na nafasi ya kuandaa Fainali ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa msimu huu.