Baada ya kuweka Rekodi ya Kuhamasisha Mashabiki kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kupanda Treni inayofanya safari zake kutoka Kamata-Pugu jijini Dar es salaam, Klabu ya Simba SC imejipanga kuendeleza mpango huo kwa Kuhamashisa Mashabiki kwa kupanda Pantoni.

Simba SC wamepanga kufanya Kampeni hiyo kwa mara nyingine, ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa mashabiki kuelekea mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, utakaopigwa Jumapili (April 17) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema wamejipanga kuzindua rasmi Kampeni za kuelekea mchezo huo kesho Jumanne (April 12), katika tawi la Tunawakera na Keshokutwa watakuwa Feri kwa ajili ya kupanda Pantoni na kuelekea mpande wa Kigamboni.

“Kwasasa tumekuwa na namna mpya ya kisasa ya kuhamasisha kuwafikia mashabiki kule walipo na sisi kama Simba SC umezaa matunda makubwa.”

“Kwenye mchezo uliopita tulipanda treni na kwenye stendi ya Magufuli, safari hii tutaenda kuzindua kampeni ya hamasa kwenye tawi la Tunawakera lililopo Chang’ombe Maduka Mawili, shughuli itakuwa kesho kuanzia saa 4 asubuhi.”

“Mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu lakini pia tutakuwa na mgeni wa heshima, Simba wa Yuda, Mwina Kaduguda na tutamleta kipenzi cha Wanasimba, mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali.”

“Kesho kutwa Jumatano tutakuwa Feri Soko la Kimataifa la Samaki kabla ya kupanda Pentoni kuelekea upande wa Kigamboni, kuendelea na Kampeni ya kuhamasisha mashabiki wetu.” amesema Ahmed Ally

Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ kwa kishindo, kufuatia kisago kilichoishukia USGN ya Niger cha 4-0 Jumapili (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC ilimaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D ikiwa na alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast na USGN ya Niger zikitupwa nje ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Rais wa Ufaransa ashinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa Urais
CAF, TFF zabariki Mashindano ya Quraan kuunguruma Uwanja wa Mkapa