Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Mfumo wa Elimu nchini unahitaji maboresho zaidi ili kuleta mageuzi kwa taifa na kuhakikisha vijana wanapomaliza shule wawe na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.
Prof.Mkenda ameyasema hayo hii leo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa 30 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo amewataka kuhakikisha wanapitia Mfumo mzima wa Elimu pamoja na Sera zake ikiwemo pia Mitaala yake ili kuhakikisha taifa linanufaika na wataalamu wanaotokana na Elimu hapa nchini.
Pia amezungumzia ubora wa elimu nchini kuwa unapaswa kupitiwa upya ili kumuandaa kijana kuwa mtaalamu huku akisema kuwa elimu haijakamilika ndio maana kuna baadhi ya vijana wanamalizi hadi vyuo vikuu lakini bado hawajakidhi katika taaluma waliosomea.
“Tunahitaji kuandaa Mtaala uliokamilika, embu tujiulize sote hapa kwa nini wataalamu wetu sio wazuri?,kwa sababu elimu yetu haijakamilika haimuandai kijana katika viwango vinavyotakiwa ndio maana nawaambia kuna haja ya kupitia upya Sera na mfumo wa elimu yetu,” amesema Prof.Mkenda.
“Tuna wajibu wa kutoa wataalamu wenye ubora na sio wataalamu wengi wasio na ubora niwaambie tu ni vigumu sana Watanzania kufaidika na matunda ya wataalamu wetu kwa sababu ya mfumo wa elimu yetu,”
Akitolea mfano kada ya Udaktari Prof.Mkenda amesema kuwa watashirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha wanapata Madaktari wenye uwezo wa kutosha kwani kumekuwa na namba kubwa ya madaktari lakini bado wagonjwa wanasafiri nje ya nchi kupata matibabu wakati wataalamu wapo hapa nchini.
“Najiuliza sana hawa Madaktari wetu wangepimwa kwa mfumo kamili kabisa wa elimu hii leo tusingekuwa na safari za kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu fulani kwani tungeweza kumaliza kila kitu hapa nchini ila naamini tukibadilisha Sera na mifumo yetu naamini tutazalisha wataalamu waliokamilika ili kulisaidia taifa letu,” amesisitiza Prof.Mkenda.
Pamoja na hayo Prof.Mkenda amesema kuwa ubora wa elimu unakwenda sambamba na miundombinu bora na salama ya kujifunzia hivyo amewataka watumishi wa wizara hiyo kuhakikisha wanasimamia miradi inayoendelea ikamilike kwa wakati kwa sababu elimu ndio urithi wa vizazi vyote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Ambaye pia ni katibu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Eliamani Sedoyeka amesema kuwa baraza hilo lipo tayari katika kuhakikisha taratibu za Wafanyakazi na taratibu za uandaaji wa rasimu ya bajeti ya mwaka 2022/2023 ya wizara hiyo unaendelea kujikita katika kuwekeza kwenye maboresho ya elimu lengo likiwa ni kuwatengeneza wataalamu wenye ubora kwa ajili ya kuwasaidia watanzaina.
Naye Katibu wa CWT Deus G. Seif amesema kuwa bila kuwa na walimu wenye ubora katika Shule zetu tutaendelea kuzalisha watalaamu wasio na vigezo hivyo ni vyema kuhakikisha wanaotoa elimu kuwa na vigezo vya kutosha ili kusaidia hii taaluma inayotegemewa na taifa.
“Nataka niwahakikishie mwalimu akikosea gharama yake ni kubwa sana kuliko kosa kufanywa na daktari au Mhandisi kwa sababu unaweza kulirekebisha lakini kosa la mwalimu ni hatari sana,” amesema Deus G.Seif.
Mkutano wa 30 wa Baraza la Wafanyakazi la kujadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya wizari hiyo ya mwaka wa 2022/2023 kabla ya kupelekwa bungeni inakwenda na kaulimbiu isemayo “Sensa ya watu na makazi ni Msingi ni kichocheo cha sera Bora na Mipango Endelevu ya elimu,Sayansi na Teknolojia, Tushiriki kikamilifu.