Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limezijumuisha Zimbabwe na Kenya katika Droo ya kufuzu kwa hatua ya makundi kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023 licha ya nchi hizo kusimamishwa uwanachama na FIFA.

Kenya na Zimbabwe zimejumuishwa katika Droo hiyo itakayofanyika Aprili 19, 2022 kwa sharti kwamba adhabu yao itaondelewa angalau wiki mbili kabla ya siku ya kwanza kwa michuano hiyo inayokusudiwa kuanza Juni 2022.

Katika taarifa yake CAF imesema “Marejeleo ya Kenya na Zimbabwe kufungiwa na FIFA katika shughuli zote za soka, endapo adhabu hiyo haitaondolewa wiki mbili kabla ya siku yao ya kwanza ya mechi za mchujo; vyama vyote viwili vitachukuliwa kuwa vilimeshindwa na kuondolewa kwenye mashindano.”

Zimbabwe ilisimamishwa baada ya Serikali kuingilia masuala ya soka kufuatia Tume ya Michezo na Burudani (SRC) kusimamisha bodi ya Shirikisho la Soka la Zimbabwe (Zifa).

Kenya ilikumbwa na ghadhabu ya Fifa kufuatia kuvunjwa kwa kamati kuu ya Shirikisho la Soka Nchini humo na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Michezo, Amina Mohamed.

Serikali ya Kenya ilivunja uongozi wa juu wa FA kufuatia kile ilichokiita usimamizi mbovu wa fedha na utawala wa Nick Mwendwa.

Xavi: Tuna hasira Ligi ya Mabingwa Ulaya
Haji Manara amkataa Joash Onyango