Klabu ya Ruvu Shooting imetumia haki yake kikanuni kuuhamisha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans kutoka Dar es salaam (Uwanja wa Benjamin Mkapa) hadi mkoani Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika).

Ruvu Shooting FC ambao ni wenyeji wa mchezo huo wamefanya maamuzi hayo kwa kutumia kanuni ya kucheza michezo miwili katika Uwanja tofauti na nyumbani, miongoni mwa viwanja visivyokuwa na michezo ya Ligi Kuu [Kanuni ya 9(7)].

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPLB’ tayari imesharidhia mabadiliko hayo na sasa mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Young Africans utachezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Mei 04.

Hii ni mara ya pili kwa Ruvu Shooting msimu huu 2021/22, kuhamisha mchezo wake kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kuupelekea Uwanja usio na michezo ya Ligi Kuu, walifanya hivyo dhidi ya Simba SC kwa kucheza Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Young Africans watacheza mchezo huo katika Uwanja wa Lake Tanganyika, huku wakikumbuka matokeo ya mchezo wa mwisho kuchezwa Uwanjani hapo dhidi ya Simba SC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ wakipoteza kwa kufungwa 1-0.

Klabu nyingine zilizotumia haki ya kuhamisha michezo kwenye viwanja ambavyo havitumiki katika Ligi Kuu ni KMC FC walifanya hivyo dhidi ya Young Africans (Uwanja wa Majimaji-Songea) na Simba Simba SC (Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi-Tabora), huku Geita Gold wakiipeleka Young Africans Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Didier Gomes aiombea kheri Simba SC
Amri Kiemba: Tatizo liko wapi Simba SC kushinda nyumbani