Baada ya kuwasili jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo Jumamosi (April 16) tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho, Kocha wa Orlando Pirats, Fadlu Davis amesema wamejiandaa kucheza mchezo mgumu dhidi ya timu inayotumia vema uwanja wake wa nyumbani.
Simba SC itaikabili Orlando Pirates kesho Jumapili (April 17), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mashabiki na Wanachama wake wakiwa na matuimaini makubwa na timu yao kuibuka na ushindi.
Kocha Davids ambaye aliwahi kuitumikia Orlando kama mchezaji, amesema amejipanga na kuifuatilia vizuri Simba SC na kujua maeneo ambayo ina nguvu na mapungufu.
“Tumekuja kupambana na timu nzuri. Timu inapocheza hatua hii ni lazima uipe heshima yake. Tutacheza nyumbani kwao huku tukichukua tahadhari kubwa kwani wanapocheza kwao wanakuwa ni hatari zaidi.”
“Simba wana washambuliaji wenye kasi, hatutakiwi kufanya makosa, hivyo tumeyafanyia kazi mapungufu yao, nguvu yao ilipo, kwani hatutakiwi kufanya makosa mengi hatarishi,” amesema Kocha huyo.
Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kishindo, baada ya kuibanjua USGN mabao 4-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (April 03), matokeo yaliyoifanya klabu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, ikitanguliwa na RS Berkane ya Morocco.
Simba SC ilifikisha alama 10 sawa na RS Berkane, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikipata alama 09 na USGN ya Niger ikikusanya alama 05 zilizoiweka mkiani mwa kundi hilo.