Aliyeendesha Mfumo wa VAR kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Orlando Pirates Termo Martin ametoa ufafanuzi wa maamuzi ya Penati iliyowanufaisha wenyeji kupata ushindi wa bao 1-0.
Simba SC ilipata mkwaju wa Penati dakika ya 66, baada ya Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison kuangushwa eneo la hatari na beki wa Orlando Pirates Happy Jele.
Dar24 Media imezungumza na Termo Martin na kumuuliza uhalali wa Mkwaju wa Penati ambao ulilalamikiwa na wachezaji wa Orlando Pirates hasa baada ya Mwamuzi Haythem Guirat kutoka Tunisia, kuamuru mkwaju huo kupigwa moja kwa moja kabla ya kupata uhakika wa VAR, lakini baadae alifanya hivyo kwa kuwasiliana na timu iliyokua ikiendesha mfumo huo.
Martins amesema alijiridhisha kupata picha za tukio la Penati na kuthibitisha wazi ilikua adhabu sahihi dhidi ya Oralndo Pirates na ndio maana mwamuzi aliamuru mchezo kuendelea, baada ya kupata uhakika kutoka chumba cha VAR.
“Kwa mchezo huu wa Simba na Orlando kulikua na tukio moja tu la Penati, na nilihakikisha ninapata picha zote ili kujiridhisha na nilijiridhisha ilikua Penati halali, ndio maana Mwamuzi aliendelea na kazi yake kwa kuamuru mkwaju ule upigwe.” amesema Martins
Kuhusu Changamoto Martin amesema: “Kwangu haukuwa mchezo wenye changamoto nyingi, ulikua mchezo wa kawaida na yaliyotokewa ni ya kawaida katika soka, nilifanya majukumu yangu ya kuhakikisha napata picha ya kila upande na nilifanya hivyo kwa usahihi kabisa.”
“Kwa mchezo huu tulitumia Kamera nane, na hii inatokana na uwezekano wa kituo kinachorusha matangazo kwa kushirikiana na CAF kinatumia Kamera ngapi (unaweza kutumia Kamera 20 hadi 35), lakini katika mchezo huu tulitumia nane pekee.”
Termo Martin amelazimima kutoka ufafanuzi huo kupitia Dar24 Media, kufuatia Kocha wa Orlando Pirates Mandla Ncikazi kulalamika kuwa Simba SC ilibebwa na Mwamuzi kwa makusudi, na ana uhakika adhabu ya Penati haikustahili dhidi ya timu yake.
Mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Simba SC dhidi ya Orlando Pirates utakaochezwa Jumapili (April 24), bado utakuwa chini ya ungalizi wa VAR kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
‘CAF’ ilitoa taarifa hiyo juma moja lililopita kwa kusisitiza michezo yote kuanzia Hatua ya Robo Fainali hadi Fainali katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho Barani Afrika itakua chini ya uangalizi wa VAR.