Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho huenda akaikabili Simba SC Jumamosi (April 30), baada ya kuanza mazoezi akiwa katika kambi ya Young Africans Avic Town, Kigamboni Jijini Dar es salaam.
Aucho kwa kipindi kirefu alikua majeruhi, lakini kukosekana kwake hakukuleta madhara yoyote kwenye kikosi cha Young Africans ambacho msimu huu kinaonekana kuwa na ari kubwa ya kushindana.
Mjumbe wa Kamati ya Usajili Young Africans Heri Said amesema kiungo huyo alianza mazoezi na wenzake tangu Jumamosi (April 16), baada ya kukosekana kwa muda mrefu.
Hersi amesema mchezaji huyo ameonesha kuwa tayari kupambana kama ilivyokua kabla hajaumia, hivyo amewataka Mashabiki na Wanachama wa Young A fricans kumsubiri Uwanjani na kuona ni vipi anaisadia klabu yao.
“Wachezaji wanaumia, wachezaji ni Binaadamu, na wanapoumia ni lazima tufuate utaratibu wa kitabibu unaotolewa kwa mchezaji anayeumia, Juzi (Jumamosi) ameanza kufanya mazoezi na wenzake.”
Kuhusu uzushi kuwa Aucho alikua na matatizo na Uongozi wa Young Africans, Hersi amesema taarifa hizo sio za kweli, na huenda zilitengenezwa kwa lengo la kuitoa klabu yao kwenye reli ya kupambana msimu huu.
“Haya mambo sijui kwa nini yanatengenezwa, sijui kwa maslahi ya nani, lakini hayana afya. Young Africans imeshavuka huko kwenye Propaganda za kitoto kwamba mchezaji ana shida na klabu, hajalipwa na mambo mengine, huko tumeshavuka.”
“Young Africans ina mkataba na mdhamini wake, anayewalipa mishahara wachezaji kwa wakati na anatoa sapoti kubwa kwa kila kitu, haya mambo yanapaswa kupuuzwa kwani yameshapitwa na wakati.” amesema Hersi.
Young Afrika inaoyongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 51, itakabiliana na Simba SC (Bingwa Mtetezi) yenye alama 41 Jumamosi (April 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.