Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ismail Aden Rage amewataka wachezaji wa klabu hiyo kuwa makini kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC Jumapili (April 24) itacheza mchezo huo Uwanja wa Orlando, huku ikiwa na kibarua cha kulinda ushindi wake wa bao 1-0, ama kusaka ushindi zaidi, ili kutinga Hatu ya Nusu Fainali.
Rage ameeleza kuwa, Wachezaji wa Simba SC wana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo huo, ili kukamilisha mpango waliouanza Dar es salaam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (April 17).
Rage amesema ana matumaini makubwa na Simba SC kufanya vizuri, endapo Wachezaji watacheza kwa kujituma na kutambua umuhimu wa kitakachowapeleka Afrika Kusini.
“Mchezo kwa hakika utakua mgumu sana, wale Orlando hawatakubali kutolewa kwenye haya mashindano, kwa hiyo wachezaji wetu wanapaswa kuwa waangalifu sana kwa kucheza mpira wa kujituma na kufuata maelekezo ya kocha wao.”
“Binafsi nina imani timu yangu ya Simba SC itaweza kupita kwenye hatua hii, lakini hili litatimia endapo kila mchezaji atajua thamani na uzito wa Jezi atakayoivaa siku ya mchezo, na kuwafikiria watanzania wanataka nini kutoka kwao.” amesema Rage
Katika mchezo wa Jumapili (April 24), Simba italazimika kulinda ushindi wake wa bao moja ama kusaka ushindi mwingine ugenini ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Nusu Fainali, huku Orlando Pirates wakihitaji ushindi kuanzia mabao mawili kwa sifuri ili kutimiza lengo la kusonga mbele.