Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Francis Baraza ameelezea kiu yake ya kuipeleka Kagera Sugar kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao wa 2022/23.

Tanzania itaendelea kuwakilishwa na timu nne kwenye michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, kufuatia klabu ya Simba SC kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho msimu huu.

Baraza amesema amejipanga kuipeleka timu yake kwenye michuano hiyo kwa kutumia nafasi ya Tanzania kuwa na uwakilishi wa timu nne kimataifa msimu ujao.

Amesema zoezi la kufanikisha mpango huo lipo mikononi mwake na kwa wachezaji wake, kupitia michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia msimu huu.

Amesema endapo Kagera Sugar itashinda michezo yote iliyosalia, itakua na nafasi nzuri ya kuingia kwenye nafasi nne za juu na kupata nafasi ya kuwa mwakilishi wa Tanzania kimataifa.

“Mahesabu yetu ni kumaliza nafasi nne za juu, ninajua kuna timu nyingi zina malengo kama haya, lakini kwetu tunajipanga ili kufanikisha hili kutokana na ubora wa kikosi changu.”

“Haitakua rahisi lakini wachezaji wangu wanafahamu kiu yetu ya kutaka kushiriki michuano ya Kimataifa, kutokana na Tanzania kuwa na nafasi nne kwenye michuano hiyo, ninaamini Kagera Sugar itakua miongoni mwa timu zitakazokwenda Kimataifa msimu ujao.”

“Mzunguuko wa pili ni wa kujitoa muhanga zaidi, kwa sababu ndio umaamua timu Bingwa na nyingine zitakazokwenda kuwakilisha nchi kimataifa, kwa hiyo kwa kutambua umuhimu huo hatutaacha kutumia nafasi tulionayo kwa sasa. amesema Kocha huyo kutoka nchini Kenya.

Katika Michezo 20 iliyocheza msimu huu, Kagera Sugar imeshinda sita, imefungwa sita na kutoka sare michezo minane huku ikishika nafasi ya tano katika Msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 26.

Ahmed Ally aziita Azam FC, Young Africans Kimataifa
Full story kisa cha kukamatwa Mpenzi wa Rihanna