Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa ufafanuzi kuhusu Jiwe la Madini ya Ruby lenye uzito wa kilo 2.8 lililoonekana Dubai ambalo linasadikika kutoka Tanzania na kueleza kuwa, wizara inaendelea kufuatilia ukweli wa taarifa zake na endapo itapata nyaraka kuhusiana na jiwe hilo kama limetoka Tanzania, Taratibu na Sheria za Tanzania zitatumika katika kupata haki ya Tanzania.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mkinga Dunstan Kitandula ambaye alitaka kujua jinsi gani Tanzania itanufaika na jiwe hilo.
Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, jiwe hilo linalosemekana kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 120 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 240 za kitanzania, taarifa zake zilionekana zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wizara ilipata taarifa zake tarehe 13 Aprili, 2022.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo, wizara ilichukua hatua za haraka ili kujua kama habari hizo ni za kweli kwa kuanza kufanya ufuatiliaji kwa kuangalia taarifa za usafirishaji wa madini ya aina hiyo kwenye kanzidata zake na kubaini kutokuwepo kwa taarifa zinazofanana za jiwe hilo kwa uzito na thamani.
Akizungumzia mmliki halali wa jiwe hilo, amesema inasemekana huenda yupo nchini Marekani katika Jimbo la California na katika ufuatiliaji wa kupata chanzo halisi na asili ya jiwe hilo, nchi tatu (3) zinahusishwa ikiwemo Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu-Dubai na Tanzania.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa wizara inawahakikishia watanzania kwamba itaendelea kusimama imara katika kudhibiti na kulinda rasilimali za watanzania kwa manufaa ya nchi hiyo.
Inaelezwa kuwa, jiwe hilo linatarajiwa kuwekwa kwenye mnada wa mauzo ya madini baada ya mfungo wa Ramadhan kuisha na baada ya kutembezwa ili kuoneshwa katika maeneo mbalimbali katika Falme za kiarabu-Dubai.