Benchi la Ufundi la Orlando Pirates limeonesha kuwa na ahuweni kufuatia kukosekena kwa Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Bernard Morrison, katika mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika utyakaopigwa kesho Jumapili (April 24).
Simba SC kesho itakua na kibarua kizito cha kuikabili Orlando Pirates ugenini, huku ikiwa na mtaji wa ushindi wa bao moja, walioupata nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (April 17).
Kocha Mkuu wa muda wa Orlando Pirates Fadlu Davids amesema kukosekana kwa Morrison kwenye mchezo huo, itakua na uafadhali mkubwa kutokana na umahiri wake ambao uliwasumbua kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza jijini Dar es salaam.
“Morrison tunamfahamu nafikiri ubora wake ni kitu kinachojieleza hata ukiangalia alivyowasaidia katika mechi iliyopita kuna mashambulizi mawili bora ambayo Simba waliyafanya kwa kila kipindi na yote yalifanywa na Morrison , kukosekana kwake katika mechi hii ni kitu muhimu kwetu ingawa nasema bado tunatakiwa kuwa makini na wachezaji wengine.”
Morrison mwenye mabao matatu na asisti nne katika michuano hiyo, ndiye aliyesababisha penati iliyoimaliza Orlando jijini Dar es Salaam iliyokwamishwa kimiani na Shomary Kapombe.
Wakati makocha wa Orlando wakiwa matumbo joto, mwenzao Pablo Franco leo Jumamosi (April 23), anatarajiwa kukamilisha Program ya maandalizi ya kuelekea mchezo huo, katika Uwanja wa Orlando baadae jioni.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania jana Ijumaa (April 22) aliendelea na Program ya mazoezi ya kikosi chake baada ya kuwasili Afrika Kusini, katika viwanja vya Highlanders.