Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Malawi na Klabu ya Simba SC Peter Banda amesema yupo tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC leo Jumapili (April 24) itakua ugenini Johannesburg-Afrika Kusini, ikisaka nafasi ya kucheza Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku ikihitaji sare ama ushindi wa aina yoyote.
Banda ambaye ni sehemu ya kikosi kilichosafiri hadi Johannesburg, amesema pamoja na kutarajia upinzani mzito kutoka kwa Pirates, Simba SC ipo tayari kukabiliana na kila kitu ili kufanikisha azma ya kupambana na kupata matokeo.
Amesema wapinzani wao wana uwezo mkubwa kisoka, lakini pia Simba SC ina hadhi kama hiyo na ndio maana imefika hatua ya Robo Fainali na mpaka sasa inaongoza kwa bao moja, walilolipata nyumbani Dar es salaam, Jumapili (April 17).
“Ni mchezo mgumu lakini jambo la muhimu ni tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huu ambao tuko ugenini. Orlando Pirates ni timu nzuri ila tumejipanga kufanya kazi ya ziada ili tuweze kusonga mbele.” Amesema Banda
Bao pekee la Simba SC dhidi ya Orlando Pirates katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza lilifungwa kwa mkwaju wa Penati kupitia kwa Beki wa Pembeni Shomari Salum Kapombe, kufuatia Bernard Morrison kuangushwa eneo la hatari.