Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Balozi. Dkt. Wilbroad Slaa, amesema katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, chama hicho kikuu cha upinzani kilimuandaa Samwel Sitta kuwa mgombea urais.
Dkt. Slaa amesema hayo katika mahojiano maalumu na Dar24 Media yaliyofanyika nyumbani kwake na kuzungumzia maisha yake kwa ujumla, Siasa alizozifanya pamoja na masuala ya kijamii.
Amesema kuwa yeye hakuwa amejiandaa kugombea na wala hakuwa na mpango wa kuwa Rais katika maisha yake, lakini kwakuwa mipango ya Chadema kumuandaa kumpa kijiti Mzee Sitta ilishindikana, aliteuliwa ghafla kuwa mgombea.
“Sisi CHADEMA wakati huo mwaka 2010 tulianza kuandaa mgombea wetu tangu Januari, na mimi nilipewa kazi ya kumuandaa mgombea wa Urais, wakati huo nikiwa Katibu Mkuu na pia nikiwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na nilifanya kazi zangu kwa uaminifu na uadilifu mkubwa bila kujiwekea kuwa nafasi hiyo nitaenda kuichukua mimi,” Dkt. Slaa aliiambia Dar24 Media.
“Ilikuwa Mheshimiwa Samweli Sitta awe mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema; na mipango yote ilikamilika. Kwa bahati mbaya mipango hiyo ilifeli dakika ya mwisho mwezi Julai karibia na kipindi cha kupiga kura ya kupitisha bajeti ya 2010/2011. Sasa mimi nilishtukishwa na Kamati Kuu kuwa baada ya hapo mgombea wetu wa Chadema atakua Dkt. Slaa. nilishtuka, niliugua na nililala siku mbili mbele naumwa,” aliongeza.
Akiendelea kufafanua zaidi kuhusiana na suala hilo la kuwa Rais, Dkt. Slaa amesema kuwa aliipokea na kujiandaa kwa kuwa alikua amepitia Ubunge kwa miaka 15 hivyo siasa aliziweza ingawa hakuwahi kuwa na tamaa ya kutaka kuwa Rais katika harakati zake siasa.
Hata hivyo Dkt. Slaa amesema kwa sasa hana shughuli nyingine bali ameamua kupumzika, kutafakari masuala ambayo ameyapitia katika maisha yake.
“Kama nilivyosema tangu naachana na CHADEMA, mimi sasa nipo huru sifungamani na chama chochote, nipo huru, na mimi sasa nina Furaha na nipo huru kusema kile ambacho ninataka kusema kuhusu nchi yangu,” amesema Dkt. Slaa.
“Kutumikia Taifa ni mpaka pale unapoingia kaburini hivyo kama kutatoea nafasi ambayo itanitaka kutumikia taifa bila kujihusisha na chama niko tayari na umri wangu haunizuii, ingawa mimi tangu nilipojitoa Chadema niliamua kujitoa kwenye siasa za vyama, na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huwezi kuwa kiongozi yoyote kama huna chama cha siasa. Lakini hiyo kitu sasa muda wake umeisha kwangu,” Dkt. Slaa aliiambia Dar24 Media.
Pamoja na maelezo hayo Dkt. Slaa ameandika kitabu ambacho bado hakijasambaa sana kinachoitwa ‘Nyuma ya Pazia: CHADEMA livyosalitiwa mwaka 2015’.
Msomi huyo amesema kwa sasa haoni tatizo kwa Serikali ya sasa kwa kuwa inaendelea kufuata nyayo za kufungua Dunia na kusaidia wanyonge.