Uongozi wa klabu ya Kiyovu FC ya Rwanda umekanusha taarifa za kufanya mazungumzo na Young Africans inayotajwa kuwa mbioni kumsajili kiungo Abeid Bigirimana kwa msimu ujao 2022/23.
Young Africans juma lililopita walitajwa kuwa kwenye mazungumzo na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Rwanda, huku Mjumbe wa Kamati ya Usajili Hersi Said na Kocha Msaidizi Cedrick Kaze walionekana wakimfuatilia mchezaji Abeid katika moja ya michezo ya Ligi ya Rwanda.
Katibu Mkuu wa Kiyovu FC Omar Gisesera amesema taarifa hizo sio za kweli na kwa sasa hawana mpango wa kuanza mazungumzo na klabu yoyote, kutokana na jukumu kubwa la ushiriki wao kwenye Ligi Kuu ya Rwanda.
Amesema taarifa za Young Africans kuhusishwa na mpango wa kumsajili Abeid sambamba na kuzungumza na Uongozi wa Kiyovu FC, wameziona zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, lakini ukweli ni kwamba hakuna lolote lililofanyika baina ya pande hizo mbili.
“Suala la sisi kuwa na mchezaji mzuri na kuhusishwa na klabu nyingine kubwa kama hapo Tanzania ni jambo zuri, lakini kwa sasa hatuna mpango wowote wa kuzungumza na klabu nyingine ama kumuuza mchezaji.”
“Kwa sasa tunaangalia sana michezo ya Ligi Kuu ya hapa Rwanda, kwa sababu tuna malengo yetu kwa msimu huu, hivyo ni mapema sana kwa sasa kuingia kwenye mpango wa kufanya mazungumzo ya kumuuza mchezaji ambaye anahitajika kwa msaada kwenye klabu hii.”
“Ikitokea tutafanya mazungumzo tutawaambia tunachokihitaji, na kama tutakubaliana biashara itafanyika, kama itashindiakana basi tutabaki na mchezaji wetu.”
Kuhusu kufika kwa Viongozi wa Young Africans na kuonekana uwanjani wakimfuatilia mchezaji Abeid Bigirimana, Omar Gisesera amesema hawafahamu lolote kuhusu hilo.
Amesema kama walifika Rwanda kwa ajili ya kumtazama mchezaji Abeid, wanajua Uongozi wa Young Africans watafuata utaratibu wa kuwasilisha ofa ili kuangalia kama wataweza kufanikiwa kumsajili Abeid.
“Hatujui lolote kama walikuja hapa, na kama walifika basi tunafahamu klabu ya Young Africans inajua nini cha kufanya kama wanamtaka mchezaji, watume maombi ya kumsajli halafu tutazungumza. Amesema Omar Gisesera
Young Africans imeanza mpango wa kukiboresha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na Michuano ya Kimataifa ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku wakilikaribia taji la Ligi Kuu msimu huu 2021/22.