Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amejivunia kikosi chake kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC kwa kusema wapo kamili, huku wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri.

Simba SC itaikabili Young Africans Jumamosi (April 30) Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiachwa kwa alama 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, jambo ambalo sio rafiki kwao, katika kutetea ubingwa walioushikilia kwa misimu minne mfululizo.

Kocha Nabi amesema kikosi chake kimeanza maandalizi kikiwa katika kamili, huku akitarajia kumtumia beki wake Dickson Job aliyempumzisha kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC ambao walikubali kufungwa mabao 2-1 Jumamosi (April 23).

Amesema hadi sasa mchezaji ambaye yupo katika hati hati za kuwepo ama kutokuwepo kwenye mchezo dhidi ya Simba SC ni Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza ambaye alikuwa majeruhi.

“Tunaingia katika maandalizi ya mechi ya Simba tukiwa na kundi kamili la wachezaji, tulimpumzisha Job (Dickson) kutokana na alikuwa na kadi mbili za njano kama angepata kadi ingetupa shida, lakini Feisal (Salum) na Aucho (Khalid) nimefurahi jinsi walivyorejea na kucheza kwa utimamu mzuri.

“Mtu aliyebaki ni Saido (Said Ntibazonkiza) ambaye naamini tunapoingia kambini leo atakuwa tayari kwa mchezo huo, huyu ni mchezaji mkubwa ambaye ni muhimu kuwa naye katika mechi kubwa kama hii inayokuja.” amesema Kocha Nabi

Young Africans imekua klabu pekee msimu huu iliyokaa kileleni kwa muda mrefu pasina kushuka, huku ikiwa imejikusanyia alama 54 baada ya kucheza michezo 20, huku Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwa kufikisha alama 41 ikiwa imecheza michezo 19.

ASAP na Rihanna waonekana na furaha licha ya kukamatwa kwake
Edo Kumwembe: Afrika tumeshindwa kutumia VAR