Klabu ya Young Africans imetakiwa kutenga Dau la Dola Laki Mbili ($200,000), endapo watahitaji huduma ya Kiungo kutoka nchini Burundi na klabu ya Kiyovu FC Abeid Birimana kwa msimu ujao wa 2022/23.
Young Africans inatajwa kumuwania kiungo huyo, huku Mjumbe wa Kamati ya Usajili Hesri Said akitajwa alifanya safari ya kwenda Kigali Rwanda sambamba na Kocha Msaidizi Cedick Kaze kwa ajili ya kumfuatilia Abeid Bigirimana.
Katibu Mkuu wa Kiyovu FC Omar Gisesera amesema thamani ya Abeid kwa sasa ni zaidi ya Dola Laki Mbili ($200,000), na kama Young Africans watakua tayari basi wanatakiwa kufahamu mazungumzo ya usajili wa mchezaji huyo yataanzia hapo na kuendelea.
Amesema Mchezaji huyo amewahi kuhusishwa na klabu kadhaa za Barani Afrika na klabu kutoka ukanda wa kiarabu, lakini Uongozi wa Kiyovu FC uliweka msimamo wa kutomuuza chini ya Dola Laki Mbili ($200,000).
“Kama Young Africans wapo tayari kutoka Dola Laki Mbili ($200,000), tupo tayari kufanya mazungumzo na kisha kuidhinisha biashara ya kuuzwa kwa Abeid, kwa sababu klabu nyingi zimewahi kuleta ofa mezani lakini hazikufika hapo tunapopahitaji.”
“Kuna Klabu moja kutoka Ukanda wa Kiarabu iliwahi kuja na ofa ambayo inakaribia na hapo lakini Uongozi wa Kiyovu FC ulishikilia msimamo wake wa kuhakikisha unamuuza Abeid Bigirimana kwa Dola Laki Mbili ($200,000).” amesema Gisesera.
Young Africans imeanza mpango wa kukiboresha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na Michuano ya Kimataifa ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku wakilikaribia taji la Ligi Kuu msimu huu 2021/22.