Mama mzazi wa mchekeshaji maarufu kutoka nchini Marekani Chris rock kwa mara ya kwanza amezungumza kuhusu kitendo cha Will Smith kumchapa kofi mtoto wake wakati wa hafla ya utolewaji wa tuzo za Oscar 2022.
Katika mahojiano yake na NBC Rose Rock amesema kuwa kofi hilo halikumuumiza mwanawe pekee bali kitendo cha Will kumpiga mwanae ni sawa na kuipiga familia yake nzima.
“Alipompiga Chris, alitupiga kofi sote, ni kama alinipiga kofi mimi, Sijui ni kitu gani ningemwambia kama ningekuwa karibu yake, umemtandika mwenzako kibao?.
”Nadhani mengi yangeweza kutokea, vipi kama Chris angeweza kurudi nyuma na kuanguka?, naamini mwisho wa siku Will Smith angeishia kutiwa pingu, hafikirii hilo?”.
”Nachojua ni kuwa ulimuitikia mke wako baada ya kukutazama na jicho la kando na ukaenda kumpiga mwenzio, kwa sababu mwanzo ulionyesha kucheka punde baada ya Chris kutoa mzaha kuhusu Jada Pinket ” amesema Rose Rock
Ameongeza kuwa ilimlazimu kufika nyumbani kwa mwanaye muda mfupi baada ya hafla ya utolewaji wa tuzo za Oscar kukamilika.
Itakumbukwa, Smith alimpiga kibao Chris Rock baada ya Rock kufanya mzaha uliomhusu mke wake, Jada Pinkett, kwa kudokezea kuonekana kwa Pinkett Smith katika filamu mpya ya “G.I. Jane” kwa sababu ya muonekano wa nywele zake.
Hata hivyo, Smith aliomba radhi na kujitetea kwa kusema kuwa alishindwa kujizuia kutokana na mzaha huo kumuhusu mke wake Pinkett ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa alopecia, ugonjwa ambao husababisha nywele za mtu kupukutika.
Tangu wakati huo, Smith ambaye alishinda tuzo ya Oscar kutokana na ushiriki wake katika filamu maarufu ‘King Richard’ aliamua kujiuzulu kutoka ‘Academy of Motion Picture Arts and Sciences’, na baadaye shirika liliamua kumsimamisha kuhudhuria sherehe za Oscar kwa takribani miaka 10.
Bodi ilimeamua na kuweka wazi kuwa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia tarehe 8 Aprili 2022, Will Smith hataruhusiwa kuhudhuria matukio au programu zozote za Oscar.
Mpaka sasa mhanga mkuu wa tukio hilo Chris Rock hajazungumza chochote, isipokuwa alidokeza kwa uchache akiwa katika onyesho lake la vichekesho kuwa utafika wakati ambao atatoa taarifa kamili kuhusu tukio hilo.
“Bado ninashughulikia kile kilichotokea,” aliuambia umati uliojitokeza kwenye tamasha lake la vichekesho Wilbur huko Boston mnamo Machi 30 2022.