Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 3, 826 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya muungano wa Tanzania.
Hayo yameelezwa katika taarifa aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, imeeleza kuwa msamaha huo unaenda sambamba na masharti mbalimbali ikiwa ni pamoja na wafungwa wote kupunguziwa robo ya vifungo vyao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 48(1) cha Sheria ya Magereza.
“Wafungwa hao sharti wawe wametumikia robo ya vifungo vyao na wawe wameingia gerezani kabla ya Februari 26, 2022 isipokuwa walioorodheshwa katika sharti la 2(1-11),” imeeleza taarifa hiyo.
Wafungwa wengine watakaonufaika na msamaha huo ni wale wenye magonjwa ya kudumu waliothibitishwa na jopo la waganga chini ya mwenyekiti mganga mkuu wa mkoa au wilaya na wawe wametumikia robo ya vifungo vyao.
Waziri Masauni amewataja wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi ambao wametumikia robo ya vifungo vyao na wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na watoto wanaonyonya, wasionyonya na wajawazito ambao wametumikia robo ya vifungo vyao pia ni miongoni mwa wanufaika wa msamaha huo.
Wengine waliopata msamaha ni wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 30 na kuendelea.