Licha ya kulalamikia halikua bao halali kwa kigezo cha Mfungaji alikua ameotea kabla ya kuukwamishwa mpira wavuni, Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limetangaza Bao la Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Orlando Pirates Kwame Peprah kuwa Bao Bora la wiki.
Peprah aliifungia Orlando Pirates bao hilo muhimu kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Simba SC ya Tanzania Jumapili (April 24).
Picha ya VAR zilionyesha Mshambuliaji huyo alikua amezidi lakini Mwamuzi Bernard Camill kutoka Visiwa vya Shelisheli aliamuru kuwa Bao halali na baadae kuzua mjadala katika mitandao ya kijamii hususan upande wa wadau wa soka la Bongo.
Bao la Peprah limetangazwa kuwa Bao Bora la wiki, baada ya kuyashinda mabao mengine yaliyofungwa katika michezo ya Hatua ya Robo Fainali iliyochezwa Jumapili (April 24), katika nchi za DR Congo, Morocco na Libya.
Mabao mengine yaliyoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania bao Bora la wiki ni lile lililofungwa na Haythem Layoun wa Al Masry akifunga dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Bao la Japhte Bola Kitambala wa TP Mazembe alilofunga kwenye mchezo dhidi ya Pyramid ya Misri nalo liliingia kwenye kinyang’anyiro hicho, huku Ayoub Ayed wa Al Ahli Tripoli bao lake dhidi ya Al Ittihad nalo liliwania nafasi hiyo.