Moja ya taarifa ya kusisimua kwa mashabiki wa mwanamuziki kutoka nchini Nigeria Wizkid ni pamoja na ripoti iliyotolewa na waandaji wa tamasha la Rolling Loud ambao wameuarifu umma kuwa wamemlipa msanii huyo kiasi cha fedha kisichopungua $1M ambazo ni sawa na zaidi ya Bilioni 2.3 za Tanzania ili kutumbuiza kama mmoja wa wasanii vinara kwenye tamasha hilo litakalofanyika huko Toronto Canada mapema Septemba 2022.
Rolling Loud ilitangaza tamasha lake la kwanza kabisa litakalofanyika nchini Canada Jumanne Aprili 26. Na tamasha la hip hop linalotazamiwa kufanyika Septemba 9-11 huko Ontario Place katikati mwa Toronto huku waimbaji wakuu ‘headliners’ wakiwa ni Dave, Future pamoja na Wizkid.
Gumzo kubwa kutoka kwa wadau mbali mbali wa muziki barani Afrika kupitia kwenye mitandao ya kijamii ni kuhusu safari ya mafanikio ya mwanamuziki Wizkid ambayo kwa sasa imemuweka kwenye viwango vya juu katika orodha ya wasanii wenye kulipwa fedha nyingi zaidi kwenye matamasha mbali mbali huku kubwa likiwa hili la Rolling Loud.
Tamasha hili limemfanya kuweka kibindoni zaidi ya shilingi Bilioni 2.3 kama malipo huku kiasi hicho cha pesa kikitajwa kuwa sawa na wanacholipwa nyota wengine wakubwa kutoka nchini Marekani akiwamo Future pamoja na Travis Scott.
Pamoja na uwepo wa orodha ya nyota hao, mashabiki watakaohudhuria tamasha hilo watapata nafasi ya kuwashuhudia wakali wengine kama Lil Uzi Vert, Migos, Skepta, Central, pamoja na mkali wa Afrobeats Rema.
Muendelezo wa tamasha hilo kwenye maeneo mengine utakuwa na nyota wengine wenye kufanya vizuri kwenye kiwanda cha muziki duniani akiwamo Ye, Future pamoja na Kendrick Lamar wakitajwa kama Headliner hii itakuwa Jully 22-24.
Ukimuweka pembeni YE, Future pamoja na Kendrick Lamar wiki moja iliyopita waliweka wazi taarifa za ujio wa albamu zao mpya ambazo zinatarajiwa kutoka katika tarehe zilizorandana na muendelezo wa tamasha hilo.
Album ya Future iitwayo ‘I Never Liked You’ itaachiwa rasmi Aprili 29, na albamu ya Lamar, ‘Mr. Morale & The Big Steppers’ iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, itatoka ifikapo Mei 13.