Aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la soka nchini TFF Michael Richard Wambura amesema Young Africans ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu, kutokana na tofauti kubwa ya alama iliopo kati yao na Mabingwa watetezi Simba SC.
Young Africans itakua mwenyeji wa Simba SC Jumamosi (April 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 54, ambazo zinaifanya kuwaacha watani zao kwa alama 13.
Wambura ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania ‘FAT’ kwa sasa Shirikisho ‘TFF’, amesema tofauti ya alama iliopo baina ya miamba hiyo ya Soka la Bongo ni sawa na kupoteza michezo mitatu hadi minne, jambo ambalo haliwezi kutokea upande wa Young Africans ili kuipa ahuweni Simba SC.
“Alama 13 ambazo wanazidiana na Simba SC ni nyingi sana, kuziba alama hizo ni michezo mitatu ama minne, Young Africans itatakiwa kupoteza na Simba SC ishinde michezo yote, sioni Young Africans ikipoteza michezo mitatu ama minne, ila bado michezo ni mingi lolote linaweza kutokea ila itakuwa maajabu,”
“Simba SC walikuwa bize Kimataifa, huku Young Africans walikua makini katika kujipanga kushinda michezo yao ya Ligi Kuu, ndio maana unaona tofauti imekua kubwa sana katika msimamo, lakini kama Simba SC nao wangekua katika michuano ya Ligi pekee yake, naamini mambo yangekua tofauti.
Wambura kwa sasa amefungiwa kujishulisha na soka, baada ya kukutwa na hatua ya kwenda kinyume na taratibu za mchezo huo pendwa duniani kote.