Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amewataka Wakuu wa Idara za Tehama Serikalini kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumika katika Taasisi zao iboreshwa ili kuweza kubadilishana taarifa ifikapo tarehe 30 Septemba, 2022 kupitia mfumo wa Serikali wa Ubadilishanaji Taarifa (GovESB).
Mhagama ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi kwa Wakuu wa Idara za Tehama Serikalini.
Pia, amesema Serikali imeweka msukumo mpya katika kutekeleza Serikali Mtandao kwa kusisitiza ushirikiano na matumizi ya pamoja ya rasilimali za TEHAMA miongoni mwa Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na kuboresha taratibu za utendaji kazi kwa kila taasisi.
“Aidha, naelekeza matumizi ya Mifumo Shirikishi pale taratibu za utendaji kazi za Taasisi za Umma zinapokuwa zinafanana badala ya kila Taasisi kuwa na Mfumo unaojitegemea.
“Naelekeza kuwa, Mifumo tumizi yote ya Serikali ihifadhiwe katika Vituo vya kuhifadhia Mifumo vilivyoidhinishwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (Approved Government HostingEnvironment),” amesema Mhagama.
Hata hivyo amesema kuwa kila taasisi ihakikishe kuwa inahifadhi Mifumo yake katika vituo mbadala (Disaster Recovery Site) vinavyofanya kazi ili kuwa na uhakika wa kuendelea kutoa huduma pale inapotokea hitilafu kwenye kituo kikuu (Primary Site).
Mhagama amesema ili kuhakikisha TEHAMA inatoa mchango chanya katika uendeshaji na usimamizi wa majukumu ya Serikali, jitihada mbalimbali zimefanyika na mafanikio yamepatikana katika maeneo ya Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo.
“Nimesikia kutoka kwa mawasilisho yaliyotangulia kuwa, pamoja na mafanikio tuliyoyapata, eneo hili bado linakabiliwa na changamoto kadhaa za kiutekelezaji, zikiwemo: Kutoshabihiana kati yataratibu za utendaji kazi Serikalini (business processes) na teknolojia inayotumika.
Waziri Mhagama ameelekeza kufanyiwa kazi haraka kuhakikisha Sheria, Kanuni, Viwango, na Miongozo ya SerikaliMtandao inazingatiwa na kufuatwa.
“Kulisisitiza hili, nawaelekeza Maafisa Masuuli wote wa Taasisi za Umma kuhakikisha kuwa idara za TEHAMA katika Taasisi zao zinaimarishwa na kuwa na watalaam wenye weledi, vitendea kazi vya kutosha pamoja na Muundo wa Usimamizi wa TEHAMA unaokubalika,” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw.Hassan Kitenge,amesema kuwa maboresho ya Utumishi wa Umma yamefanyika katika eneo la sera na mifumo ili kuongoza utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao.
“Utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni moja ya maeneo muhimu ya maboresho yaliyofanyika katika Utumishi wa Umma, ambao umesaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa Umma,” amesema Kitenge.
Awali Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kuwa e-GA, ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kusimamia, kukuza jitihada za Serikali Mtandao na kuhimiza uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha Taasisi za Umma zinatumia TEHAMA kwa usahihi na Usalama.
Hivyo Mhandisi Ndomba amesema kuwa ni wajibu wa Wakuu wa Idara/Vitengo vya TEHAMA Serikalini kusimamia utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika Taasisi zao kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao iliyopo.
”Sheria ya Serikali Mtandao inahimiza matumizi sahihi na salama ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na kuwa na Mifumo inayowasiliana na kubadilishana Taarifa. Katika kufikia lengo hilo, Mamlaka imeandaa Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao,” amesema Mhandisi Ndomba.
Hata hivyo amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kuwa wasikivu lakini pia kuwa tayari kutoa maoni yao pale itakapohitajika ili waweze kufikia lengo la uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao wakati wa utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao kwenye Taasisi zao.