Mwili wa Rais Mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki umeondoka hii leo saa moja asubuhi katika Hifadhi ya Maiti ya Lee kuelekea nyumbani kwake Othaya katika Kaunti ya Nyeri.
Mwili wa Kibaki umeendelea kufunikwa kwa bendera ya Kenya, kuwekwa kwenye gari la kubeba maiti na kusindikizwa na maafisa wa jeshi kwa mfano wa msafara wa rais.
Mwili huo uliwekwa katika kigari cha kubeba bunduki ukiwa umbali wa mita 400 kufika kwenye eneo kulikoandaliwa misa ya mazishi huku familia ya Kibaki ikiwa kwenye msafara huo na Rais Uhuru Kenyatta akiratibiwa kuongoza hafla ya kumuaga rais huyo wa tatu wa Kenya.
Wananchi wa Maeneo mbalimbali walionekana wamekusanyika kando ya barabara kuangalia jeneza lilobeba mwili wa aliyekuwa rais wao na kumpa heshima zao za mwisho.
Huko Othaya, wananchi tayari wamewasili katika shule ya Othaya Approved kulikoandaliwa hafla ya mazishi ya Kibaki kabla ya mwili wake kusafirishwa hadi kwenye boma lake kwa mazishi.
Kusafirishwa kwa mwili huo kwa barabara ni moja ya matakwa ya aliyokuwa nayo Hayati Kibaki kabla ya kifo chake na Mwili huo utazikwa nyumbani kwake katika hafla ya kibinafsi baada ya familia kuomba usiri wakati wa mazishi.