Kikosi Young Africans kimeondoka jijini Dar es salaam mapema leo Jumatatu (Mei 02) kuelekea mkoani Kigoma tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting.
Young Africans imesafiri kuelekea Mkoani Kigoma kwa usafiri wa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, huku ikiwa na kikosi kamili ambacho kiliikabili Simba SC Jumamosi (April 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana.
Ruvu Shooting ambao ni wenyeji wa mchezo huo, waliamua kuchagua Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo mkoani Kigoma, kwa kuzingatia kanuni za Ligi Kuu, ambazo zinatoa nafasi kwa klabu shiriki kucheza michezo isiyozidi miwili kwenye viwanja tofauti na uwanja wake wa nyumbani.
Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara imesafiri na matumaini makubwa ya kuendelea kutoa dozi kwa klabu za Ligi Kuu, baada ya kushindwa kufanya hivyo dhidi ya Simba SC Jumamosi (April 30).
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, Young Afrucans iliibamiza Ruvu Shooting mabao 3-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mabao ya wababe hao wa Jangwani yakifungwa na Feisal Salum, Djuma Shaban na Mukoko Tonombe huku bao la maafande wa Ruvu likifungwa na Shaban Msala.
Mara ya mwisho Young Africans kucheza Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ilikua ddhi ya Simba SC katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzanzania Bara ‘ASFC’, ambapo klabu hiyo Kongwe nchini ilikubali kichapo cha bao 1-0, likifungwa na Kiungo kutoka nchini Uganda Tadeo Lwanga.