Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire amesema umewadia wakati wa kikosi cha Young Africans kuondoka Uwanjani vichwa chini, baada ya Simba SC kushindwa kufanya hivyo Jumamosi (April 30).
Tambo hizo za Masau Bwire, zimechukua nafasi kufuatia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utazikutanisha Ruvu Shooting na Young Africans keshokutwa Jumatano (Mei 04), mkoani Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika.
Masau Bwire amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo na wamedhamiria kuwathibitishia mashabiki wa soka la Bongo wao ndio itakua timu ya kwanza kuibuka na ushindi dhidi ya Young Africans.
“Kocha wetu Boniface Mkwasa ameshawajenga vijana katika hali ya kisaikolojia, na sisi viongozi tumethibitisha hilo kwa sababu tupo pamoja na kila mmoja kwenye timu yetu, hivyo tunaamini Young Africans wanakwenda kuinamisha vichwa vyao chini baada ya mchezo.”
“Naweza nikawa nazungumza haya, lakini ninafahamu kuna watu wananibeza kwa kusema ninajifurahisha, ila niwakikishie tupo vizuri kwa ajili ya kupambana na kuifunga Young Africans keshokutwa, tumeleta mchezo huu Kigoma kwa kusudi la kuwafurahisha mashabiki wetu huku, na hakuna lingine zaidi ya kuifunga hii timu ambayo inasifika haijafungwa tangu msimu huu ulipoanza.” amesema Masau Bwire
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, Young Afrucans iliibamiza Ruvu Shooting mabao 3-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mabao ya wababe hao wa Jangwani yakifungwa na Feisal Salum ‘FEI TOTO’, Djuma Shaban na Mukoko Tonombe huku bao la Maafande wa Ruvu likifungwa na Shaban Msala.