Ndoto za Mabingwa Watetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara Wekundu wa Msimbazi Simba za kukutana na Young Africans kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Michuano hiyo bado zinaendelea kuishi, licha ya kukabiliwa na mchezo wa Robo Fainali dhidi ya Pamba FC ya jijini Mwanza.

Simba SC itacheza dhidi ya Pamba FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara May 14 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, baada ya mchezo huo kuahirishwa kufuatia Mnyama kuwa na majukumu ya Kimataifa mwezi uliopita.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema wanatamani kukutana na Young Africans katika hatua ya Nusu Fainali, kwa kuamini bado wana deni la kuifunga timu hiyo msimu huu 2021/22, baada ya kushindwa kufanya hivyo katika michezo ya Ligi Kuu iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana.

“Hii ngoma bado ‘MBICHI’, kwa sababu tunaaini kwa yoyote atakayekua na kikosi bora katika michezo iliyosalia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, ndio atakua bingwa.”

“Kwa sisi kama Simba SC bado tumewekeza nguvu kwenye Ligi Kuu, ila nguvu zaidi tumewekeza kwenye Kombe la Shirikisho na huo ndio mfumo wa maisha ulivyo, kuna wakati inakulazimu kuwekeza nguvu kwenye mahala ambapo una nafasi kubwa ya kwenda kupata mafanikio.”

“Kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, Simba SC ina nafasi kubwa ya kwenda kuchukua ubingwa wa Kombe hilo, kwa hiyo akili, mawazo na nguvu yetu yote tunaelekeza kwenye michuano hii, tumejipanga kumalizana na Pamba FC kwanza, tumnyoe Mwananchi halafu tuchukue Ubingwa.”

“Msimu huu Simba SC ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho, ndio itakua klabu ambayo imepata mafanikio zaidi kuliko klabu nyingine yoyote.” Amesema Ahmed Ally

Simba SC msimu uliopita ilitawazwa kuwa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, baada ya kuifunga Young Africans bao 1-0, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Kabla ya hapo msimu wa 2019/20, Simba SC iliitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuichabanga Namungo FC mabao 2-1, Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Young Africans ilifanikiwa kupenya hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho kwa kuichapa Geita Gold FC kwa changamoto ya mikwaju ya penati, baada ya timu hizo kwenda sare ya bao moja kwa moja ndani ya dakika 90.

Timu nyingine zilizotinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho ni Azam FC ikiitoa Polisi Tanzania kwa kuifunga mabao 3-0, pamoja na Kagera Sugar ikiibanjua Coastal Union kwa changamoto ya mikwaju ya penati 5-4, baada ya kwenda sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

Kwa mantiki hiyo Azam FC itacheza dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho, huku Young Africans akimsubiri mshindi wa mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Pamba FC ya Mwanza.

TARURA yaondolewa kukusanya ushuru wa maegesho
J Melody awachana wasanii madalali