Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa nchini (TAKUKURU), Salumu Hamduni kukutana Jumatatu ijayo Makao Makuu ya Ofisi za Bohari ya Madawa (MSD).
Kukutana kwa viongozi hao itakuwa ni kushughulika na waliofanya udanganyifu wa zabuni za ununuzi vifaa tiba kwa ajili ya hospitali za serikali.
Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi Mei 5, 2022 jijini Arusha, wakati akifungua wiki ya Manunuzi ya Umma, iliyohudhuriwa na wataalamu 1,003 wa sekta hiyo kutoka serikalini, taasisi binafsi na wadau mbalimbali.
Amesema serikali haitaaacha salama watendaji hao na wale wenye kutumia hovyo taaluma yao kwa kula fedha za walipa kodi, kwa kujinufaisha wao.
Amesema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonesha jinsi baadhi ya watendaji wa MSD walivyofanya udanganyifu wa kuongeza maradufu ununuaji wa vifaa tiba hospitali za serikali katika zabuni.
‘’IGP na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru tukutane MSD Jumatatu tukashughulike na wale wenye tamaa ya kula fedha za walipa kodi bila ya aibu,” amesema Waziri Mkuu.