Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza FC Mbwana Makata ametoa pongezi kwa wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyoifanya dhidi ya Tanzania Prisons jana Alhamis (Mei 05), Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma mjini Songea.
Mbeya Kwanza FC iliyokuwa mwenyeji wa mchezo huo, iliibanjua Tanzania Prisons bao moja kwa sifiri, na kuendelea kuweka hai matumaini ya kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2022/23.
Makata aliyekabidhiwa kikosi cha Mbeya Kwanza FC baada ya kuondoka Dodoma Jijini FC, amesema hana budi kusema ahsante kwa wachezaji wake, kutokana kutimiza wajibu wao wa kupambana uwanjani na kupata ushindi huo.
Amesema siri kubwa iliyopelekea kuifunga Tanzania Prisons Jana Alhamis, ni umoja na mshikamano uliopo kikosini kwake sambamba na kufuata maelekeo ya Benchi la Ufundi.
“Ninashukuru timu inaendelea kubadilika siku hadi siku, na nina imani huko mbele kutakua na mambo mazuri, tunapambana ili kuendelea kupata matokeo mazuri yatakayo tuwezesha kuwa katika mahala salama.”
“Wachezaji wangu kwa ujumla wamejituma sana, kwa hilo ninawashukuru na kuwapongeza, umoja na mshikamano walionao ndio chachu ya matokeo haya, pamoja na kufuata maelekezo yangu pamoja na wenzangu katika Benchi la Ufundi.” amesema Mbwana Makata
Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, umeiwezesha Mbeya Kwanza FC kufikisha alama 21, zinazoiweka nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu, huku Tanzania Prisons ikibaki nafasi ya 14 kwa kuwa na alama 22.