Msemaji wa klabu ya Young Africans Haji Sunday Ramadhan amesema kikosi cha klabu hiyo kimeanza kujipanga kuelekea mchezo wa mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu dhidi ya Maafande wa Jeshi la Megereza ‘Tanzania Prisons’.
Young Africans iliyorejea jana Alhamis (Mei 05) jijini Dar es salaam ikitokea mkoani Kigoma, itakua mwenyeji wa mchezo huo Jumatatu (Mei 09), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Manara amesema kikosi chao kimeanza maandalizi, na Benchi la Ufundi limejipanga kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo miwili iliyopita iliyoshuhudia wakitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Simba SC kisha Ruvu Shooting.
Amesema mpango mkuu kwa sasa ni kuhakikisha kikosi chao hakirudii makosa ya kuangusha alama, na watahakikisha Tanzania Prisons inakua timu ya kwanza kuirudisha timu yao katika ramani ya ushindi.
“Tutacheza kwa kuiheshimu Tanzania Prisons, tumekubali matokeo ya michezo iliyopta tumetoka sare ya bila kufungana, lakini mchezo wetu wa Jumatatu, makocha watapambana kwa kushirikiana na wachezaji ili tuweze kuibuka na alama tatu Insha Allah.” amesema Haji Manara
Young Africans inaendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 56, huku ikiwa timu pekee katika Ligi hiyo ambayo haijapoteza mchezo kwa msimu huu 2021/22.