Serikali ya Somalia imetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais wa taifa hilo ulioshindwa kufanyika 10/10/2021 kutokana na ghasia sasa utafanyika 15/5/2022.
Runinga ya taifa nchini Somalia, imetangaza taarifa ya kamati ya bunge iliyopewa jukumu la kuandaa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Mjumbe wa kamati ya uchaguzi wa bunge Mohamed Ibrahim Moalimu, ameandika katika mtandao wake wa Facebook kuwa, wanachama wa kamati hiyo kwa kuzingatia hali ya sasa ya nchi hiyo wamekubaliana Mei 15 kuwa siku ya uchaguzi wa rais.
Uchaguzi huo ambao umecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, umekumbwa na mzozo wa kuonyeshana ubabe wa madaraka kati ya rais Mohamed Abdullahi anayejulikana kama Farmajo, na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble.
Washirika wa kimataifa wa Somalia wamekuwa wakishinikiza mchakato huo wa uchaguzi ufanyike haraka, wakihofia kucheleweshwa kwa uchaguzi huo kutakwamisha pia juhudi za kukabiliana na matatizo mengine ikiwemo vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabab na tishio la baa la njaa.