Rais wa Marekani, Joe Biden amemteua Karine Jean-Pierre kuwa msemaji mkuu wa Serikali na ataanza kazi kuanzia wiki ijayo.

Karine Jean-Piere anakuwa mwanamke wa kwanza mweusi kushika wadhifa huo katika historia ya Marekani.

Jean-Pierre (44), anachukua nafasi inayoachwa wazi na Jen Psaki anayetajwa kujiunga na kituo cha utangazaji cha MSNBC.

Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa juu wa utoaji habari na majadiliano na waandishi wa habari, Karine Jean-Pierre aliwahi kuwa mnadhimu mkuu wa kambi ya Kamala Harris baada ya Harris kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Joe Biden kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani.

Uteuzi wa Karine Jean-Pierre unatajwa kuwa moja ya mkakati wa Rais Biden na makamu wake Kamala Harris kuelekea kwenye uchaguzi mdogo wa katikati ya muhula utakaofanyika mwezi Novemba ambao unatajwa kutoa taswira ya namna rais anayekuwa madarakani atakavyoweza kumaliza kipindi cha muhula wake.

Mbali ya nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika, Karine Jean-Pierre pia alikuwa msemaji mkuu wa shirika la utetezi la MoveOn wakati wa uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2016.

Mtangulizi wake wa nafasi ya msemaji mkuu wa ikulu ya Washington, Jen Psaki amemsifia Jean-Pierre kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika “mwanamke wa kupigiwa mfano mwenye maadili ya juu”.

Waziri atoa onyo kupandisha bei kiholela 'ni kosa la jinai'
Sabaya aachiwa huru