Kikosi cha Azam FC leo Jumapili (Mei 08) majira ya mchana kilianza safari ya kuelekea jijini Mbeya tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 23 wa Ligi kuu dhidi ya Mbeya City FC.
Azam FC imeondoka jijini Dar es salaam kwa usafiri wa Ndege ili kupata muda mzuri wa kujiandaa na mchezo huo, ambao unatarajiwa kuwa na vuta ni kuvute kutokana na hitaji la timu zote mbili.
Miamba hiyo itakutana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku Azam FC ikiwa na lengo la kusaka ushindi utakaoendelea kuiweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, lakini Mbeya City FC itahitaji kurekebisha makosa yaliyopelekea kupoteza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar FC jana Jumamosi (Mei 07), mkoani Morogoro.
Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Instagram wa klabu ya Azam FC imeeleza: “ #OffToMbeya Kikosi cha Azam FC mchana huu saa sita kamili kimeondoka kuelekea Mbeya.”
Azam FC imeondoka jijini Dar es salaam huku ikichagizwa na ushindi wa mabao 2-1 walioupata jana Jumamosi (Mei 07) dhidi ya KMC FC katika uwanja wa Azam Complex.
Mabao ya Azam FC dhidi ya KMC FC yalifungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Rodgers Kola, huku bao la kufutia machozi la Kino Boys likifungwa na Mshambuliaji kutoka Tanzania Miraji Athuman.