Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin amesema baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC FC jana Jumamosi (Mei 07), kazi inayofuata ni kuhakikisha anakiandaa vyema kikosi chake ili kikabiliane vyema na Mbeya City FC itakayokua nyumbani.
Miamba hiyo itakutana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku Azam FC ikiwa na lengo la kusaka ushindi utakaoendelea kuiweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, lakini Mbeya City FC itahitaji kurekebisha makosa yaliyopelekea kupoteza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar FC jana Jumamosi (Mei 07), mkoani Morogoro.
Kocha Abdihamid Moallin amesema amemalizana na KMC FC na sasa anakwenda Mbeya kupambana kuzisaka alama tatu nyingine, huku akitambua wenyeji wao wapo katika hali ya kuhitaji matokeo, kufuatia kushindwa kufanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya Kwanza FC.
“Najua hautakua mchezo rahisi kwetu na kwao pia, lakini kwa upande wangu kama Kocha wa Azam FC nitajitahidi kikosi changu kipambane kama ilivyokua kwenye mchezo wa jana dhidi ya KMC FC, na tupate alama tatu nyingine zitakazoendelea kutuweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.”
“Kwa sasa michezo ya Ligi Kuu imekua na changamoto kubwa ya ushindani, na hii ni kutokana na kila timu inahitaji kupata ushindi ili kufikia malengo yake, na sisi kama Azam FC tuna malengo yetu, hivyo hatutachoka kupambana hadi tufikie lengo letu.”
Mabao ya Azam FC dhidi ya KMC FC yalifungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Rodgers Kola, huku bao la kutufia machozi la Kino Boys likifungwa na Mshambuliaji kutoka Tanzania Miraji Athuman.