Kiungo Mshambuliaji wa Ruvu Shooting Abdul-Swamadu Kassim amesema bado ana ndoto za kurudi Simba SC, baada ya kuondoka kwenye klabu hiyo wakati wa Dirisha Dogo la Usajili (Januari 2022).
Abdul-Swamadu alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu kama mchezaji huru, baada ya kuachwa na Kagera Sugar, lakini kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Msimbazi kulimfanya ashindwe kuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Pablo.
Kiungo huyo kutoka Visiwani Zanzibar, amesema ndoto zake kubwa ni kuendelea kucheza soka katika kiwango cha juu, na anaamini hilo ndilo litakalomuwezesha kurudi ndani ya Simba SC ama kwenda klabu nyingine yenye viwango vya juu katika Ligi ya Tanzania Bara.
“Soka ni mchezo mpana ambao kila siku unaonekana hadharani, mimi nina ndoto za kurudi Simba ama kucheza popote pale ambapo patakua na hadhi kubwa kama ya Simba SC, sijakata tamaa.”
“Ninaamini nia uwezo mkubwa na dhamira ya kufikia ndoto zangu ninaendelea kuifanyia kazi kwa vitendo, sitachoka kwa sababu mimi ni mchezaji na ninapata nafasi ya kucheza nikiwa Ruvu Shooting.”
“Kocha wa Simba SC niliwahi kuzungumza naye wakati ule tulipocheza nao kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, aliniambia mambo mengi sana na kuniaminisha bado nina nafasi ya kurudi kwenye kikosi chake kama nitafikia kiwango anachohitaji, hata wakati ninaondoka Simba SC aliniambia hivyo hivyo, sina haraka ninaamini yatatimia.” Amesema Abdul-Swamadu Kassim
Kiungo huyo alikua sehemu ya kikosi cha Ruvu Shooting kilichoecheza jana dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuambulia kisago cha mabao manne kwa moja.