Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya DTB FC itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2022/23 Muhibu Kanu, amesema haikuwa rahisi kwao kufanikisha lengo hilo, kutokana na ushindani mkubwa waliokutana nao kwenye Mshike Mshike wa Ligi Daraja la Kwanza.

Muhibu Kanu amesema ugumu wa ushiriki wa DTB FC kwenye Ligi Daraja la kwanza ulitokana na mfumo wa Ligi moja uliotumika msimu huu tofauti na ilivyokua misimu ya nyuma ambapo timu ziliwekwa kwenye makundi mawili tofauti.

Amesema kwa uzoefu wake na ushirikiano na Viongozi wengine wa DTB FC, imekua siri kubwa ya kufikia lengo la kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, kufuatia kuwa sehemu ya mapambano ya Ligi Daraja la Kwanza.

“Wakati nikiwa Pamba FC msimu uliopita nilijifunza mambo mengi sana, hadi ninaondoka pale kuna baadhi ya mambo niliona ndio chahu ya mafanikio katika Ligi Daraja la Kwanza, nilipokuja DTB FC nilitumia changamoto hizo kama sehemu ya kuwashawishi viongozi.”

“Niliwaambia viongozi wa DTB FC lazima wawekeze kwa kiasi kikubwa na kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa hali ya juu, nashukuru hilo walilitimiza kwa vitendo, na ndio maana mliona wachezaji wenye kaliba ya juu ya kushindana walisajiliwa na ndio hao hao wameiwezesha timu hii kufika hapa ilipo.”

“Wachezaji kama Amis Tambwe, Juma Abdul, David Mwantika, Nicolus Gyan, Yusufu Mlipili na wengine wengi, hawa wote inakuonyesha ni vipi tulivyokua na lengo la kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza, ninamshukuru Mungu tumefanikiwa.” amesema Muhibu Kanu.

DTB FC ilijihakikishia kupanda Ligi Kuu kwa kuichapa Pamba FC bao 1-0 juzi Jumapili (Mei 08) uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam na kufikisha alama 65 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu nyingine kwa sasa isipokua Ihefu FC.

Ihefu FC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 62, huku michezo miwili ikisalia kwa timu shiriki kwenye michuano hiyo kwa msimu huu 2021/22.

Mshindi wa kwanza na wa pili kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza wanapanda Moja kwa Moja Ligi Kuu kwa msimu ujao, huku mshindi wa tatu na wa nne watasubiri kucheza michezo ya Play Off dhidi ya timu za Ligi Kuu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14.

Simba SC yalamba Milioni 50 Kombe la Shirikisho
Ahmed Ally aipiga kijembe Young Africans