Serikali imesema itaendelea kuongeza jitihada katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na wizara husika ili kuhakikisha makundi hayo yanakuwa salama.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakati akiongoza kikao cha Kamati Elekezi ya Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma kikihudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali na wadau wa maendeleo nchini.
Katibu Mkuu huyo amesema ipo haja ya kuongeza nguvu katika mapambano hayo kila mdau kwa nafasi yake ili kuongeza jitihada za utekelezaji wa mpango huo kutokana na kuongezeka kwa vitendo na matukio ya ukatili katika maeneo mbalimbali.
“Inabidi tuongeze nguvu yaani Serikali, Wizara za kisekta , Idara,Taasisi, Asasi za kiraia, wadau na vyombo vya ulinzi katika mapambano haya wote kwa nafasi zetu ili kuongeza kazi ya utekelezaji wa mpango huu na kufikia hilo lazima tuwe na rasilimali kulinda na kutetea makundi ambayo yamekuwa yakiathirika kutokana na vitendo hivyo,”alisema Dkt. Jingu.
Pia ameongeza kwamba kwa mujibu wa muongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 unaelekeza kutengwa kwa fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za MTAKUWWA huku akiziomba taasisi na wadau kuona namna ya kuongeza rasilimali kufikia malengo ya Serikali ya kukomesha vitendo vya ukatili.
“Wenzetu wadau wa maendeleo na Asasi za kiraia nimewaomba tuongeze rasirimali katika vita hii kwa sababu inahitaji ushirikiano wa pamoja kwani inamgusa kila mmoja wetu katika jamii zetu itatusaidia kutatua changamoto zinazokabili juhudi hizi na pia mnaweza kuajiri vijana wenye fani za masuala ya maendeleo ya jamii au zinazofanana na haya mambo kuongeza kasi ya mapambano,” alibainisha Katibu Mkuu huyo.
Aidha Mtaalamu wa Masuala ya Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Bi. Vailet Mollel ameeleza kwamba kwamba wamekuwa wakitoa elimu katika jamii namna ya kudhibiti vyanzo vya ukatili huku akiahidi kwama shirika hilo litaendelea kuunga mkono Serikali katika uandaji wa mkakati mpya wa 2022/2027 pamoja na kuratibu kamati za ulinzi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa.
“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali hatutaishia hapa tulipo na kuwajengea uwezo wataalamu kama jeshi la polisi, wanasheria, mahakama, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii ili waweze kukabiliana na vyanzo vya ukatili kama mila kandamizi na desturi kupitia uanzishaji wa vikundi vya malezi, viongozi wa dini na viongozi wa kimila,” alifafanua Mtaalamu huyo.