Serikali imeuelekeza uongozi wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania ambayo inajenga meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu kuzingatia makubaliano yote yaliyomo kwenye mkataba wa ujenzi wa meli hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo Mei 14, 2022 katika kikao kati yake na Balozi wa Korea ya Kusini nchini, Kim Sun Pyo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam.

Katika Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania Bw. Kwak ambaye alikiri mapungufu katika utekelezaji wa mradi huo na aliahidi kuwa kampuni yake itaongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa wakati na meli hiyo iweze kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye kikao na Balozi wa Korea na Uongozi wa Gas Entec

Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza kuwa watalaamu wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania warejeshewe Pasi zao za kusafiria ambazo zilizuiwa na Serikali kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mwenendo wa ujenzi wa meli hiyo.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Mbarouk Mbarouk na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Fred Mwakibete.

Wengine ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za meli, Philemon Bagambilana na Kanali Samwel Mahirane ambaye ni Kamishina wa Uhamiaji, Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka nchini.

Liverpool yaibanjua Chelsea, yatwaa Kombe la FA
UNAIDS yapongeza jitihada za Serikali kukabiliana na Ukimwi