Kampuni ya Gas Entec Tanzania inayojenga meli mpya ya “MV Mwanza Hapa Kazi Tu” imeomba radhi kwa Serikali kutokana na mapungufu ambayo yamejitokeza.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Dong Myung Kwak alikiri mapungufu yaliyojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huo mbele ya Balozi wa Korea Kusini hapa nchini, Bw. Kim Sun Pyo kwenye kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mei 14, 2022, Bw. Kwak aliahidi kuwa watarekebisha kasoro zote zilizojitokeza ikiwemo kuwarudisha wafanyakazi waliowapunguza kazini.
Pia aliahidi kuwa wataendelea na kazi na kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa wakati na meli hiyo iweze kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.
Kufuatia ombi lao la msamaha, Waziri Mkuu alielekeza watalaamu hao warejeshewe pasi zao za kusafiria ambazo zilizuiwa na Serikali kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mwenendo wa ujenzi wa meli hiyo.
Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Jamhuri ya Korea Kusini, na akawataka wataalamu hao wazingatie makubaliano yote yaliyomo kwenye mkataba wa ujenzi wa meli hiyo.