Watanzania wametakiwa kulinda miundombinu ya nchi pamoja na ile ambayo ipo kwenye miradi ya maendeleo ya unjenzi wa Barabara na reli ili kupata fursa za ajira na kujiendeleza kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan hii leo Mkoani Tabora alipohutubua wananchi wakati akiamalizia ziara yake mkoani humo.

“Natoa rai kwenu kuendelea kuilinda miundombinu yote, miundombinu inapokuja ni fursa za ajira hivyo, naomba mchangamkie fursa hizo vinginevyo wanaofanya kazi katika miradi hiyo wakikosa huduma wataagiza kutoka maeneo mengine,” amesema.

“Nawaahidi Wananchi wa Tabora kuwa Serikali itaendelea kutekeleza huduma zote za kijamii, hatutoacha kitu bali tutaendelea kutekeleza ili wananchi wapate huduma wanazostahiki,” aliongeza Rais Samia.

Amesema Serikali katika utekelezaji huo, haitomuacha mtu nyuma, katika kufikia maendeleo, kama ilivyoagizwa kwenye malengo endelevu ya Dunia kwamba Nchi inapokwenda na maendeleo ichukue haja za watu wote na isimuache mtu nyuma.

Ameongeza, “Tanzania ya miaka ijayo itakuwa na sura tofauti kabisa kimaendeleo kwani tunaenda kuiendeleza Tanzania, natoa rai kwa Mawaziri kuchapa kazi kwa maendeleo ya nchi,”

Hata hivyo Rais Samia amewaomba wote wanaosimamia fedha za Halmashauri kusimamia vyema kwa kuzipeleka fedha hizo kufanya kazi zilizokusudiwa, na kuwaonya watakaomjaribu. “wale wanaotaka kunijaribu wanijaribu.”

Rais Samia alikuwa ziarani Mkoani Tabora kwa siku tatu akikagua miradi ya maendeleo na leo amehitimisha ziara hiyo kwa kuhutubia wananchi.

Rubani mwanamke mtoto atua Kenya na 'Chombo'
Rais Samia asisitiza kilimo cha Alizeti na Mchikichi kunusuru hali ya mafuta