Kiongozi wa zamani wa Guinea Alpha Conde (84), amesafiri kuelekea nchini Uturuki baada ya Serikali ya kijeshi iliyompindua kuidhinisha safari yake nje ya nchi kwa ruhusa maalum ya matibabu.
Kwa mujibu wa afisa wa usimamizi wa uwanja wa ndege na afisa wa polisi Conde alipanda ndege iliyokuwa ikielekea Uturuki katika uwanja wa ndege wa Conakry asubuhi na kudai kiongozi huyo alionekana kuondoka bila usaidizi wa kiitifaki.
“Conde amepewa ruhusa kwa heshima ya hadhi na uadilifu wake na sababu za kibinadamu za kiafya,” taarifa ya Polisi imeeleza.
Hata hivyo taarifa hiyo haijaeleza hali ya Conde ingawa imebainisha kupata rufaa ya matibabu nje ya nchi huku Kamati ya Kitaifa ya mikutano na Maendeleo ikishindwa kutoa maelekezo kuhusu utaratibu wa matibabu na muda gani angekuwa nje ya nchi.
Guinea mapema mwezi huu ilifungua uchunguzi wa kimahakama dhidi ya Conde na maafisa wengine kadhaa juu ya mauaji, utesaji, utekaji nyara, uporaji na ubakaji wakati wa utawala wake.
Moja ya sababu zinazotajwa kusababisha Conde kupinduliwa ni maamuzi yake ya kupitisha katiba mpya mwaka 2020 iliyokuwa ikimruhusu kuwania muhula wa tatu wa urais.
Hata hivyo kutokana na kushikiliwa kwa tuhuma mbalimbali zinazomkabili hatimaye Aprili 22, 2022 ilitolewa taarifa kuwa Conde ameachiliwa huru lakini hakuonekana hadharani tangu wakati huo.
Awali alizuiliwa na baadaye kuruhusiwa kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa matibabu mwezi Januari 2022 na akarejea Guinea mapema mwezi Aprili 2022.
Maafisa wa jeshi wakiongozwa na Kanali Mamady Doumbouya walimpindua Conde Septemba 2021 baada ya kukaa madarakani kwa miaka 11 katika nchi hiyo koloni la Ufaransa.